Wakazi wa Mtube walia na changamoto ya nyumba zao kujaa maji
19 May 2021, 1:50 pm
Na; Shani Nicolous
Wakazi wa mtaa wa Mtube Kata ya Nkuhungu jijini Dodoma wameelezea changamoto wanazokutana nazo kufuatia makazi yao kujaa maji wakati wa msimu wa mvua na kulazimika kuhamishiwa katika makazi ya muda.
Wakizungumza na taswira ya habari wakazi hao wamesema kitendo cha maji kujaa kwenye makazi kimesababisha hali ya maisha kuwa ngumu ikiwa ni pamoja na wanafunzi kushindwa kwenda shule.
Wamesema hivi sasa wamekuwa wakihangaika kutafuta nyumba za kupanga licha ya ukosefu wa fedha kutokana na kutojipanga na suala hilo.
Aidha wameiomba Serikali iwapatie msaada ili waweze kukabiliana na changamoto hiyo ambayo inawakabili kwa muda mrefu sasa.
Dodoma fm imezungumza na Mwenyekiti wa mtaa huo Bw. John Masaka ambaye amesema Serikali inalojukumu la kuwaisaidia wananchi hao ikiwa hakuna uwezekano wa kuyatoa maji hayo basi watafutiwe makazi mengine ya kudumu.
Tukio hilo la kujaa maji katika mtaa wa Mtube Kata ya Nkuhungu jijini Dodoma lilitokea Januari 14, 2020 ambapo kaya zaidi mia moja zilizungukwa na maji ambayo yameendelea kuwepo hadi leo.