Changamoto ya maji safi na salama kata ya Ipagala yapata ufumbuzi
18 May 2021, 1:08 pm
Na; Shani Nicolous
Baadhi ya wanawake katika Mtaa wa Swaswa Mnarani , Kata ya Ipagala jijini Dodoma wamechanga fedha kwa ajili ya kuchimba kisima ili kukabiliana na changamoto ya maji inayowakabili kwa muda mrefu.
Wakizungumza na Dodoma fm wanawake hao wamesema kuwa shughuli ya kutafuta maji ni ya kwao kama wanawake hivyo wamelazimika kuchangishana pesa ili kutatua changamoto hiyo.
Hata hivyo licha ya kunufaika na maji hayo lakini yameonekana kukosa usalama kwa matumizi ambapo wamesema wanapoyatumia kuogea hutokewa na upele mwilini.
Nae mwenyekiti wa Mtaa huo Bw.Charles Nyuma amekiri kuwepo adha hiyo na tayari alishafanya jitihada za kufuatilia katika mamlaka ya maji na usafi wa mazingira DUWASA wakaahidi kuitatua.
Dodoma fm imezungumza na Sebastian Warioba ambaye ni afisa uhusiano DUWASA ambapo amewatoa hofu wananchi hao kwa kuwa wapo katika marekebisho ya kutatua baadhi ya changamoto kwa jiji zima la Dodoma ili kuongeza wingi wa maji.
Jitihada zimekuwa zikifanywa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maji kutafuta ufumbuzi wa rasilimali hiyo ambayo imekuwa changamoto kwa maeneo mengi nchini.