Wakazi wa jiji la Dodoma wametakiwa kuzingatia ramani ya nyumba wanazo jenga zijumuishe choo bora.
7 May 2021, 1:12 pm
NA; Shani Nicolous
Halmashauri ya jiji la Dodoma kwa sasa imejikita kuhakikisha kila nyumba inayojengwa inazingatia ramani ya choo bora kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya.
Hayo yamesemwa na Afisa afya wa jiji la Dodoma Bw.Abdalah Mahiya alipo kuwa akizungumza na taswira ya habari ambapo amesema kuwa choo bora ni muhimu kwa kila kaya hivyo kwa kuendeleza kampeni ya nyumba ni choo watazingatia zaidi nyumba zinazojengwa zinakuwa na huduma hiyo.
Bw.Mahiya amesema kupitia kampeni ya kufanya usafi kila jumamosi ya mwisho wa mwezi imesaidia sana kueneza kauli ya nyumba ni choo na hata kuwafikia watu wa kila mahali Mijini na Vijijini .
Aidha ameongeza kuwa kwa kipindi kirefu jiji la Dodoma lilisumbuliwa na magonjwa ya mlipuko ukiwemo kipindupindu lakini kwa sasa magonjwa haya yametoweka ikiwa ni matokeo chanya ya kampeni hiyo.
Mahiya amewataka wananchi kutambua sifa za choo bora kwani ndiyo msingi wa afya ili kuzidi kulitengenezea hadhi jiji la Dodoma ikifuatiwa na kufanya usafi katika mazingira yanayo wazunguka.
Nao baadhi ya wananchi jijini Dodoma wamesema kuwa njia hiyo itasaidia watu kuzidi kutokomeza magonjwa ya milipuko iliyokuwa ikisababishwa na uchafu wa mazingira ikiwemo kutokuwa na vyoo bora.
Kampeni ya usafi nchini Tanzania inayosimamiwa na wizara ya afya na ustawi wa jamii yenye malengo ya kuhamasisha jamii kudumisha usafi na ujenzi wa vyoo bora imekuwa na mafanikio makubwa baada ya elimu kuifikia jamii moja kwa moja.