90,025 kuanza mitihani kidato cha sita
3 May 2021, 7:05 am
Na; James Justine
KATIBU Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dk. Charles Msonde amesema, takribani wanafunzi 90,025 wameanza kufanya mtihani wa Kidato cha Sita kuanzia leo Jumatatu tarehe 3 hadi 25 Mei 2021.
Dk. Msonde ametoa taarifa hiyo jana Jumapili tarehe 2 Mei 2021, wakati akizungumza na wanahabari mkoani Dar es Salaam.
Amesema leo tarehe 3 hadi 25 Mei 2021 kutakuwa na mitihani ya kidato cha sita pamoja na ualimu ambayo itakuwa inafanyika katika taifa letu la Tanzania Bara na Zanzibar,kwenye jumla ya vituo 804 vya shule za sekondari na 248 vya kujitegemea na vyuo vya ualimu 75.
Dk. Msonde amesema kwa upande wa mtihani wa kidato cha sita 92,500 ndiyo waliosajiliwa kufanya mtihani huo kwa mwaka huu 2021, ambapo kati yao waliosajiliwa, watahiniwa 81,343 wa shule za sekondari na 8,682 ni wanafunzi wa kujitegemea.
Katibu Mtendaji huyo wa NECTA amesema, watahiniwa 46,233 kati ya 81,343 ni wavulana huku wanawake wakiwa ni 35110.
“Tunao pia watahiniwa wenye mahitaji maalum 118 kwenye mtihani huu , kati yao 95 wenye uono hafifu na 23 wasioona. Kati ya watahiniwa wa kujitegemea 8,682, wanaume ni 5,759 sawa na asilimia 66.33 na wanawake 2,923 sawa na asilimia 33.67,” amesema Dk.Msonde.
Kuhusu mtihani wa ualimu, Dk. Msonde amesema watahiniwa 6973 wamesajiliwa kufanya mtihani huo katika kozi mbalimbali, ambapo 2,187 katika ngazi ya Stashahada na 4,786 wa ngazi ya cheti.
Aidha, Dk. Msonde amewaonya wakuu wa shule na watahaniwa kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu katika mitihani hiyo.