Wananchi waombwa kutoa ushirikiano ili kukomesha mwendokasi
9 April 2021, 9:21 am
Na; James Justine.
Mamlaka ya udhibiti usafiri ardhini LATRA imetoa ombi kwa wananchi kuendelea kutumia namba za simu zilizopo kwenye mabasi endapo dereva ataendesha gari kwa mwendo kasi wakiwa safarini.
Taarifa hiyo imetolewa na afisa mfawidhi mamlaka ya udhibiti usafiri ardhini Bw.Ezekiel Emmanuel wakati akizungumza na Taswira ya habari ambapo amesema, mamlaka inaendelea kuwakamata madereva wasiofuata sheria za barabarani ikiwepo kuendesha gari kwa mwendo kasi hivyo wanahitaji ushirikiano kutoka kwa wananchi .
Aidha ameongeza kuwa wanahitaji mchango wa wananchi haswa pale madereva wanapokuwa wamechezea kifaa cha vehicle tracking system kwani huwapoteza na kufanya washindwe kutambua gari lipo kwenye mwendo kasi kiasi gani.
Kwa upande wa wakazi wa jiji la Dodoma wametoa maoni tofauti juu ya swala la utumiaji wa namba za dharura kutoka mamlaka ya udhibiti usafiri ardhini Tanzania ambapo wamesema ni vema elimu ikatolewa kwa wananchi juu ya matumizi ya namba hizo kwani madereva wengi wamekuwa wakiendesha kwa mwendokasi lakini wananchi hushindwa kutoa taarifa mahali husika.
Bw.Ezekiel ametoa wito kwa wasafiri wa mabasi ya Mikoani wanapokwenda kukata tiketi wahakikishe wanapewa tiketi za kieletronick na sio zile za zamani zinazoandikwa kwa mkono.