Wakazi wa Matumbulu wapata neema ya umeme
6 April 2021, 12:36 pm
Na; Benald Flbert
Baada ya hivi karibuni Dodoma fm kuripoti taarifa kuhusu ukosefu wa huduma ya umeme katika baadhi ya maeneo ya Kata ya Matumburu, shirika la umeme TANESCOMkoa wa Dodoma limeanza kusambaza nguzo kwa ajili ya kuwaunganishia huduma hiyo.
Akizungumza na taswira ya habari diwani wa Kata ya Matumburu Emanuel Samson Chibago amethibitisha kupelekwa nguzo katika Kata hiyo na kinachofuata ni kuunganishiwa huduma ya umeme.
Akitaja maeneo ambayo nguzo zimeanza kutandazwa Chibago amesema ni pamoja na mtaa wa Ukombozi, Kaunda hadi Muungano.
Ameongeza kuwa kazi hiyo itakapokamilika itaibua fursa nyingi za kiuchumi kwa wakazi wa Kata hiyo ikiwemo kuanzisha viwanda mbalimbali vitakavyowasaidia watu kujiajiri.
Kadhalika amewataka wananchi kuchangamkia fursa ya kuunganishiwa umeme mara baada ya nguzo kufika katika maeneo yao ya makazi ili kuondokana na changamoto wanazokutana nazo zinazohitaji nishati hiyo.
Hivi karibuni wananchi wa Kata ya Matumburu walinukuliwa na Taswira ya habari wakilalamikia juu ya kukosa huduma ya umeme ambapo wamedai hali hiyo imechangia kuwadidimiza kiuchumi.