Shughuli ndogondogo ni chachu ya kujikwamua kwa walemavu
30 March 2021, 11:43 am
Na; Thadey Tesha
Wito umetolewa kwa watu wenye ulemavu jijini hapa kujishughulisha na kazi mbalimbali zilizopo ndani ya uwezo wao ili kupunguza utegemezi katika jamii.
Wito huo umetolewa na baadhi ya viongozi wa karakana ya watu wenye ulemavu Mkoani Dodoma KAWADO akiwemo mwenyekiti wa karakana hiyo Bw.Mwita Mwara wakati akizungumza na Taswira ya habari.
Amesema ni vyema watu wenye ulemavu wakaacha kubweteka na badala yake wajihusishe na shughuli ndogondogo ili kujiingizia kipato kuliko kukaa barabarani na kuomba.
Wakizungumzia mchango wa aliyekuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hayati Dkt.John Magufuli, mhasibu wa karakana hiyo Bw. Alex Mhando amesema hayati Magufuli alikuwa mstari wa mbele kuwasadia watu wenye ulemavu kwa kutoa mikopo huku akimuomba rais wa sasa Mh.Samia Suluhu kuendelea kuwasadia ili kuwapunguzia utegemezi.
Nao baadhi ya wananchi wa jiji la Dodoma wamesema kila mwananchi anao wajibu wa kuwasadia watu hao na kuacha tabia ya kuwanyanyapaa kutokana na ulemavu wao.
Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuwasadia watu wenye ulemavu kuwainua katika sekta mbalimbali ambapo pia ilitunga sheria ya kuwasaidia kupata mikopo pindi wanapojiunga katika vikundi.