Dodoma FM

Wafanyabiashara Gulio la Chilonwa walilia vyoo bora

23 February 2021, 3:11 pm

Na, Selemani Kodima,

Dodoma.

Usemi wa Nyumba ni choo! ambao umekuwa ukitumika katika kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha vyoo bora umekuwa tofauti katika gulio la Chilonwa Wilaya ya Chamwino Dodoma, ambapo wananchi wengi wa eneo hilo hawalipi uzito unaopaswa.

Baadhi ya wananchi wa Chilonwa wakizungumza na Taswira ya Habari hii leo, wamesema hali ya vyoo katika gulio hilo inasikikitisha na kuogopesha kutokana na baadhi ya wafanyabiashara na watu wengine kuingia vichakani kwa ajili ya kujisitiri .

Keneth Mwaluko na Adam Ndoma ni wakazi wa Chilonwa wamesema kutokana na matumizi mabaya ya vyoo na mazingira yasiyoridhisha imesababisha baadhi ya wananachi kuogopa kwenda kununua bidhaa katika gulio hilo.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Chilonwa Alpha Gilbert amesema walikuwa na mpango wa kukodisha eneo hilo lakini palitokea Mvutano baina ya wafanyabishara wa gulio hilo na Serikali ya Kijiji, hali ambayo imewalazimu kuwa na mpango wa kujenga choo ambacho kitakuwa mali ya Serikali.

Diwani Alpha amewakikishia wananchi na wafanyabiashara wa eneo hilo kuwa ndani ya miezi mitatu watakuwa wamekamilisha ujenzi wa choo katika Gulio hilo ambapo gharama za ujenzi ni Shilingi laki nane.