Mbadala wa vifungashio visivyotakiwa kupatikana
2 February 2021, 8:25 am
Na,Mariam Matundu,
Dodoma.
Kufuatia tamko la Waziri wa nchi Ofisi ya makamu wa rais Muungano na mazingira Mh.Ummy Mwalimu la Januari 8 mwaka huu kutoa muda wa miezi 3 kuhakikisha vifungashio vinavyotumika kufungia bidhaa sokoni havitumiki , watendaji wameanza kutoa wito kwa wazalishaji kuzalisha mifuko inayokidhi viwango .
Akizungumza na taswira ya habari afisa kutoka ofisi ya raisi TAMISEMI Sanford Kway amewatoa hofu wananchi kuwa baada ya siku 90 alizozitoa Waziri lazima utapatikana mbadala wa vifungashio hivyo.
Amesema wametoa muda wa siku 90 ili kuwafanya wafanyabiashara ambao tayari wana bidhaa hizo kuhakikisha zinaisha na kwamba baada ya siku hizo kutafanyika operesheni maalumu na hakutakuwa na muda wa ziada.
Aidha amesema licha ya Serikali kufanikiwa kuondoa mifuko ya plastiki sokoni bado kumeibuka wazalisha wasio wazalendo ambao wanazalisha mifuko mbadala isiyokidhi viwango vya TBS na kwamba wanaendelea kupambana nao.