Dodoma FM

Waziri wa Maji afanya ziara ya kushtukiza kukagua uchimbaji visima

21 December 2020, 2:47 pm

Na,Mindi Joseph,

Dodoma.

Waziri wa Maji Jumaa Aweso ameridhishwa na utekelezaji wa mradi wa maji wa Mzakwe wenye thamani zaidi ya milioni 200 unaotarajiwa kuzalisha maji lita laki nne kwa saa katika kuendelea kupunguza adha ya maji kwa Mkoa wa Dodoma unaokabiliwa na uhitaji wa lita milioni 103.

Waziri Aweso ameyasema hayo Baada ya kufanya ziara ya kushutukiza kukagua utekelezaji wa mradi wa maji wa Mzakwe ambapo amesema Kisima hicho kinauwezo wa kuzalisha lita laki nne kwa saa na kuendelea kutatua changamoto ya maji jijini Dodoma na amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuhakikisha vinachimbwa visima vingine vikubwa viwili.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji DUWASA ,Mhandisi, Aron Joseph amesema mradi huo unatekelezwa na Kampuni ya Shanxi na amebainisha kuwa kisima kitakuwa na urefu wa mita 150 ambapo hadi sasa kimefikia theluthi ya utekelezaji wake ambapo mradi huo ulitarajiwa kukamilika ndani ya siku 60 lakini watatekeleza kwa muda wa siku 30.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Josephat Maganga akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa ziara ya kushitukiza ya Waziri wa Maji baada ya kumaliza kukagua maendeleo ya uchimbwaji visima katika eneo la Mamba pembezoni mwa jiji la Dodoma

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi, Anthony Sanga ameahidi kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Maji na amewahimiza Watanzania kuendelea kutunza vyanzo vya maji katika maeneo yao.