Kila Halmashauri ipande miti milioni moja na laki tano
18 December 2020, 3:41 pm
Na,Mindi Joseph,
Dodoma.
Serikali imewataka maafisa mazingira wa Mikoa yote Nchini kuhakikisha Halmshauri zote zilizopo katika Mikoa yao zinapanda miti milioni moja na laki tano kila mwaka ili kuhifadhi mazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Akizungumza na Waandishi wa habari katika Uzinduzi wa jiwe la utambulisho eneo la msitu wa Jiji la Dodoma Medeli Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.Ummy Mwalimu amesema Halmashauri zote zinawajibu wa kupanda miti hiyo itakayosaidia kupunguza ongezeko la joto Nchini.
Kwa upande wake Mtaalamu wa Mazingira kutoka Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori (WWF) Dkt.Severin Kalonga amesema wamepanda miche isiyopungua elfu nne katika eneo la msitu wa Medeli na asilimia 90 ya miche imepona.
Naye Zureikha Kachwamba Afisa Misitu kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS amebainisha kuwa miti milioni 1 na lakini nane imepandwa katika jiji la la Dodoma na Miche Laki tano ipo katika Bustani na inatarajiwa kupandwa.
Katika hatua nyingine Afisa Mazingira Mkoa wa Dodoma Salvatory Mashamba amehimiza Jamii inapopanda miti kuhakikisha inakua kwa kuzingatia sheria ya jiji ya upandaji wa miti 5 kwa kila familia.
Mradi wa kukijanisha Dodoma unasimamiwa na Wadhamini wakuu ambao ni Vodacom foundation kwa kushirikiana na Serikali na wadau wengine wa mazingira WWF na TFS katika kuhakikisha Dodoma inakuwa ya kijani.
Katika hatua nyingine aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe.Mussa Azzan Zungu amekabidhi ofisi kwa waziri mteule Mh.Ummy Mwalim.
Hafla hiyo ya makabidhiano imefanyika hii leo katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.