Waziri Jafo atangaza waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza 2021
17 December 2020, 2:28 pm
Na,Mariam Matundu,
Dodoma.
Waziri wa Tamisemi Selemani Jafo amewaagiza viongozi wa mikoa kwa kushirikiana na wadau wa elimu kuhakikisha wanakamilisha miundombinu ili wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza waweze kuripoti shule mapema Januari mwaka 2021.
Waziri Jafo ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema wanafunzi 759,706 sawa na 91.15% kati ya wanafunzi 759,737 wamechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2021
Aidha ameitaja mikoa ambayo wanafunzi wamebaki na wanatarajia kupangiwa shule katika awamu ya pili .
Amesema wizara imetoa pesa za kutosha kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa ambapo zaidi ya bilioni 90 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa zaidi ya elfu moja na hivyo kuwatoa hofu wazazi kwamba kila mwanafunzi aliyefaulu atajiunga na kidato cha kwanza.
Amesema iwapo wazazi na walezi wanahoja kuhusu uchaguzi wa wanafunzi wafike katika ofisi za mikoa na halmashauri husika ili kuonana na maafisa elimu waweze kuwasaidia.
Kwa mara ya kwanza wizara ya Tamisemi imefanya uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza kwa njia ya kielektroniki ambapo kati ya waliochaguliwa wavulana ni 368,174 na wasichana ni 391,532.
Mwisho.