Dodoma FM
Dodoma FM
23 January 2026, 3:56 pm

Sheria hiyo inakataza mtu yeyote kuingia au kukaa nchini bila kibali, kuingia kwa njia zisizo rasmi au kuendelea kukaa baada ya muda wa kibali kuisha, hali inayomfanya atambulike kama mhamiaji haramu na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo faini, kifungo au kufukuzwa nchini.
Na Anwary Shabani.
Idara ya Uhamiaji mkoa wa Dodoma imesema kupitia kampeni ya “Mjue Jirani Yako”, imejipanga kuwabaini na kuwachukulia hatua kali za kisheria wahamiaji wasiofuata sheria wanaoishi nchini Tanzania kinyume na sheria za uhamiaji.
Sheria ya Uhamiaji nchini Tanzania, inayosimamiwa na Sheria ya Uhamiaji Na. 7 ya mwaka 1995, inaeleza kuwa raia wa kigeni anaruhusiwa kuingia, kuishi au kufanya shughuli zozote nchini endapo atakuwa na nyaraka halali ikiwemo pasipoti, visa au kibali cha kuishi kulingana na sababu ya uwepo wake.
Hayo yamebainishwa na Mkaguzi Msaidizi wa Idara ya Uhamiaji mkoa wa Dodoma, Pius Kabeluka, wakati akizungumza na Dodoma Fm, amesema kampeni hiyo inalenga kushirikisha jamii katika kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia kuwatambua wahamiaji wanaoingia na kuishi nchini bila vibali halali, hali ambayo ni tishio kwa usalama wa nchi.
Aidha, Pius Kabeluka ameongeza kuwa njia sahihi kwa raia wa kigeni kuingia na kuishi nchini Tanzania ni kupitia vibali halali ya masomo na vibali vya sheria.
Kwa upande wake, Konstebo Asha Mwangila kutoka Idara ya Uhamiaji mkoa wa Dodoma, amesema vibali vya raia wa kigeni wanaotaka kusihi Tanzania hutofautiana kulingana na aina ya kibali achoomba mwaombaji.
Idara ya Uhamiaji mkoa wa Dodomaimewahimiza wananchi kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kulinda usalama wa nchi kwa kushiriki kikamilifu katika kampeni ya Mjue Jirani Yako, ikiwa ni sehemu ya jukumu la kila raia.