Dodoma FM
Dodoma FM
19 January 2026, 3:33 pm

Uchaguzi wa viongozi katika soko hilo unatarajiwa kufanyika Januari 24, 2026.
Na Lilian Leopold.
Jumla ya wagombea 67 wamejitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika soko la wazi la Machinga Complex jijini Dodoma.
Nafasi zinazowaniwa ni pamoja na Mwenyekiti, Mwenyekiti msaidizi, Katibu, Katibu msaidizi, Mabalozi wa vizimba na Wawakilishi wa makundi maalum.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo Mratibu wa zoezi la uchaguzi soko la wazi la Machinga Complex Jumanne Sinoni, amesema zoezi hilo limekamilika rasmi na kuelezea kuwa hatua inayoendelea kwa sasa ni urejeshaji wa fomu.
Sinoni amewataka wagombea kuzingatia muda uliopangwa wa kurejesha fomu ili kutoa fursa ya kuzifanyia uhakiki na mchujo kabla ya kuingia hatua ya uchaguzi.
Kwa upande wao, baadhi ya wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti akiwemo,Nyamageni Kingamkono, Marko Mhagale na Mlemaga Mlemaga wameahidi kuwatumikia wafanyabiashara iwapo watapata ridhaa ya kuchaguliwa.