Dodoma FM
Dodoma FM
12 January 2026, 1:50 pm

Sanjari na hayo, Rashidi Rafael amewahimiza wananchi kuwa waaminifu, wazalendo na wawazi katika kutoa taarifa kwa vyombo husika, akisisitiza kuwa taarifa hizo zitashughulikiwa kwa mujibu wa sheria ili kulinda usalama wa jamii na taifa kwa ujumla.
Na Anwary Shabani.
Jeshi la Uhamiaji mkoa wa Dodoma linaendelea na kampeni maalum ijulikanayo kama “Mjue Jirani Yako”, yenye lengo la kuwabaini na kuwachukulia hatua wahamiaji haramu wanaoishi nchini Tanzania kinyume na sheria za uhamiaji.
Akizungumza na Taswira ya Habari, Rashidi Raphael Mwaiko, Mkaguzi Msaidizi katika Jeshi la Uhamiaji mkoa wa Dodoma, amesema kampeni hiyo inalenga kushirikisha jamii katika kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia kuwatambua wahamiaji wanaoingia na kuishi nchini bila vibali halali, hali ambayo ni tishio kwa usalama wa nchi.
Aidha, Mwaiko ameeleza kuwa njia sahihi ya raia wa kigeni kuingia nchini Tanzania ni kupitia mipaka rasmi kwa kutumia nyaraka halali ikiwemo pasipoti na vibali vya kazi au makazi, huku akisisitiza kuwa kutumia njia za panya ni kosa la kisheria.

Kwa upande wao, wananchi na wakazi wa eneo la Mwatano jijini Dodoma, wamesema uwepo wa wahamiaji haramu unaweza kusababisha athari mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa matukio ya uporaji, uvunjifu wa amani pamoja na uhalifu mwingine. Wananchi hao wameiomba serikali kuimarisha ulinzi na kuchukua hatua madhubuti .