Dodoma FM

INEC yasisitiza maandalizi ya uchaguzi yamekamilika

28 October 2025, 3:24 pm

Picha ni Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele.Picha na Tume huru ya uchaguzi.

Katika taarifa yake, Jaji Mwambegele ametoa maelekezo 10 muhimu ambayo wapiga kura wote wanapaswa kuyazingatia siku ya uchaguzi.

Na Lilian Leopold.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa maelekezo 10 kwa wapiga kura na wadau wote wa uchaguzi kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika kesho Jumatano Oktoba 29, 2025 huku ikisisitiza maandalizi yote yamekamilika na Watanzania wanapaswa kujitokeza kutekeleza haki yao ya kikatiba kwa amani na utulivu.

Taarifa hiyo ya INEC imetolewa Jumanne Oktoba 28, 2025 na Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele siku moja kabla ya uchaguzi mkuu huku akisisitiza watendaji wa vituo tayari wamepatiwa mafunzo na taratibu zote za uchaguzi zimekamilika kwa mujibu wa sheria.

Jaji Mwambegele amesema INEC imekamilisha maandalizi yote ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, na kuwaomba Watanzania wote wajitokeze kwa amani, kwa kufuata sheria na kanuni za uchaguzi, amani ya nchi yetu ni jukumu letu sote.

Katika taarifa yake, Jaji Mwambegele ametoa maelekezo 10 muhimu ambayo wapiga kura wote wanapaswa kuyazingatia siku ya uchaguzi.

Kwa wapiga kura wasiokuwa na picha, Jaji Mwambegele amesema wapiga kura ambao majina yao yapo kwenye Daftari la Kudumu lakini picha zao hazionekani, wataruhusiwa kupiga kura endapo taarifa nyingine kwenye kadi zitakuwa sahihi.

Kwa wapiga kura waliopoteza au kuharibu kadi zao wataruhusiwa kutumia kitambulisho cha Taifa (Nida), leseni ya udereva, au pasi ya kusafiria kuthibitisha utambulisho wao.

Mpiga kura mwenye kadi ambayo taarifa zake hazipo kwenye Daftari la Kudumu hataruhusiwa kupiga kura, kwani uthibitisho wa taarifa kwenye daftari ndiyo unaotambulika kisheria.

Nako kwa wapiga kura wa kata zilizofutwa, zikiwemo Kanoge, Katumba, Mishamo na Milambo, Tume imewahamishia kwenye vituo vipya vilivyoidhinishwa kuhakikisha kila mmoja anashiriki uchaguzi.