Dodoma FM

Wizara ya Habari yalaani vitendo vya ukiukwaji wa maadili mtandaoni

21 October 2025, 3:53 pm

Picha ni taarifa kwa umma kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Picha na Selemani Kodima.

Wizara imekumbusha kuwa usambazaji wa maudhui yasiyo na maadili ni kosa kisheria chini ya Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, na kwamba usambazaji huo huongeza madhara kwa jamii.

Na Selemani Kodima.

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imetoa tamko kali la kulaani vitendo vinavyokiuka maadili ya Mtanzania kufuatia kusambaa kwa picha jongevu mitandaoni zinazoonesha baadhi ya watu wakicheza ngoma na muziki usio na staha katika maeneo ya wazi, vyombo vya usafiri na makazi.

Kupitia taarifa iliyotolewa, Wizara hiyo imesema vitendo hivyo vinakiuka misingi ya maadili ya Kitanzania na vimesababisha taharuki kwa jamii, ikisisitiza kuwa maudhui hayo hayakubaliki katika jamii inayozingatia maadili na utamaduni wa Mtanzania.

Wizara hiyo imetoa wito kwa wananchi na wadau wote wenye taarifa kuhusu matukio ya uvunjifu wa maadili kutoa taarifa kwa mamlaka husika ikiwemo Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Wizara yenyewe ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.

Kwa wahusika wanaoendelea kuzichapisha picha hizo kwenye mitandao ya kijamii, Wizara imewataka kuzifuta mara moja ili kulinda maadili ya Kitanzania na kuepuka kuingia kwenye mgogoro wa kisheria.

Katika hatua nyingine, Wizara imesisitiza kuwa usimamizi wa maadili ni jukumu la jamii nzima kama ilivyoainishwa katika Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997. Imesema itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutoa elimu kwa makundi tofauti na kuchukua hatua kwa wote wanaokiuka misingi ya maadili kwa makusudi.