Dodoma FM

Makosa ya maadili, utoro na wizi yatawala rufaa 108 za watumishi wa umma

20 October 2025, 3:46 pm

Picha ni Kaimu Katibu Mkuu wa Tume ya Utumishi wa Umma John Mbisso, katika mkutano wa kwanza wa mwaka wa fedha 2025/26 uliofanyika jijini Dodoma. Picha na Selemani Kodima.

Katika mkutano wa kwanza wa mwaka wa fedha 2025/26 uliofanyika jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Hamisa Kalombola, ameendesha kikao hicho kilichojadili na kufanya maamuzi juu ya rufaa na malalamiko yaliyowasilishwa.

Na Selemani Kodima.

Tume ya Utumishi wa Umma imepokea jumla ya rufaa na malalamiko 108 kutoka kwa watumishi wa umma nchini, ambapo makosa ya ukiukwaji wa maadili, utoro kazini, kughushi vyeti na wizi wa mali za umma yametajwa kuongoza.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Katibu Mkuu wa Tume hiyo, John Mbisso, amesema kati ya rufaa 93 zilizopokelewa,34 zimekubaliwa bila masharti,9 zimekubaliwa kwa masharti ya kuanza upya kwa mamlaka za nidhamu,38 zimekataliwa,10 zimetupiliwa mbali kwa kuwasilishwa nje ya muda

Kwa upande wa malalamiko 15 yaliyowasilishwa, Mbisso amesema,6 yalikubaliwa,6 yakakataliwa,3 yakaondolewa kwa kukosa mashiko.

Sauti ya John Mbisso.

Mbisso ameongeza kuwa kada zilizowasilisha rufaa na malalamiko kwa wingi ni kutoka mamlaka za serikali za mitaa.

Picha ni Afisa Sheria wa Tume ya Utumishi wa Umma Hussein Mussa.

Kwa upande wake, Afisa Sheria wa Tume hiyo, Hussein Mussa, amesema tume ina mamlaka ya kurudisha mashauri kwa mamlaka husika endapo haki haikuzingatiwa, kwa mujibu wa kifungu cha 62(4) cha Sheria ya Utumishi wa Umma.

Sauti ya Hussein Mussa.

Katika kikao hicho, warufani 18 na warufaniwa 3 waliruhusiwa kufika mbele ya tume kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu hoja zao.

Mbisso amewakumbusha watumishi wa umma kuzingatia maadili, sheria na taratibu za utumishi ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Sauti ya John Mbisso.