Dodoma FM
Dodoma FM
8 October 2025, 2:37 pm

Uzinduzi huo umeonesha dhamira ya DUWASA kuendelea kujenga mahusiano bora na wananchi, huku ikiboresha huduma kwa kuzingatia maoni na mahitaji ya wateja wake.
Na Selemani Kodima.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph, amewataka watumishi wa mamlaka hiyo kutumia vyema Wiki ya Huduma kwa Wateja kama fursa ya kutathmini uhusiano wao na wananchi, pamoja na kukusanya maoni yatakayosaidia kuboresha huduma wanazotoa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa wiki hiyo, iliyofanyika sambamba na semina elekezi kuhusu namna bora ya utoaji wa huduma, Mhandisi Aron amesisitiza kuwa wiki hiyo haipaswi kuwa ya maonesho pekee, bali iwe jukwaa la kujifunza na kujitathmini.
Katika hafla hiyo, watumishi wa DUWASA wamempongeza Mkurugenzi huyo kwa uongozi wake mahiri unaoendelea kuimarisha utoaji wa huduma ndani ya mamlaka hiyo. Ishara ya pongezi hiyo ilijumuisha tuzo maalum iliyotolewa kwa Mhandisi Aron kutambua mchango wake katika ufanisi wa DUWASA.
Aidha, mamlaka hiyo imetumia uzinduzi huo kutoa tuzo za shukrani kwa baadhi ya watumishi na wateja waliotoa mchango mkubwa katika kuendeleza huduma za DUWASA. Tuzo hizo zilitolewa kama sehemu ya kutambua juhudi za pamoja baina ya mamlaka na jamii.

Kwa upande wa uwajibikaji wa kijamii, DUWASA pia ilitoa misaada kwa Hospitali ya Taifa ya Mirembe, ikiwa ni sehemu ya kuonesha mshikamano na kutambua mchango wa taasisi hiyo katika huduma za afya mkoani Dodoma sambamba na kuwa wadau wakubwa wa Mamlaka hiyo.
Uzinduzi huo umeonesha dhamira ya DUWASA kuendelea kujenga mahusiano bora na wananchi, huku ikiboresha huduma kwa kuzingatia maoni na mahitaji ya wateja wake.