Dodoma FM

MTAKUWWA kutoa elimu juu ya madhara ya ajira kwa watoto

26 September 2025, 3:07 pm

Picha ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri ambae pia ni mwenyekiti wa kamati ya MTAKUWWA Wilaya ya Dodoma.Picha na Dodomacctz.

Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) Halmashauri ya Jiji la Dodoma umefanya kikao kwaajili ya kuandaa mpango wa kuelimisha jamii na kuhakikisha watoto wanaenda shule na kuepuka mazingira hatarishi ya ajira zisizo rasmi.

Na Lilian Lopold.
Mkakati wa kutoa elimu juu ya madhara ya ajira kwa watoto unatarajiwa kufanyika ukiwa na lengo la kupeleka ujumbe kwa jamii ili kuachana na dhana ya kuwatumikisha watoto na badala yake wawape nafasi ya kusoma na kulinda haki zao.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri ambae pia ni mwenyekiti wa kamati ya MTAKUWWA Wilaya ya Dodoma amewataka wajumbe kupita kwenye maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kutoa elimu kwa wananchi kuhusu athari za ajira za watoto kwa mustakabali wa taifa.

Picha ni kikao cha wajumbe kupita kwenye maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma .Picha na Dodomacctz.

Naye, Makamu Askofu wa Kanisa la FPCT Jimbo la Dodoma, Mchungaji Daudi Msaghaa amebainisha kuwa taasisi za dini zimekuwa mstari wa mbele kutoa elimu dhidi ya ukandamizaji wa wanawake na watoto, jambo linalosaidia kupunguza vitendo vya unyanyasaji katika familia na jamii.

Kwa upande wake, Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Wilaya ya Dodoma (SHIVYAWATA), Bhoke Manyori amesema bado wanaendelea kufanya uchunguzi wa kina kubaini idadi ya watoto wanaotumikishwa kazi kinyume na umri wao katika Wilaya ya Dodoma.