Dodoma FM

VEO Paranga watakiwa kuwajibika kwa wananchi

26 September 2025, 12:41 pm

Picha ni Hilary Hilary, Mkuu wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba.Picha na Seleman Kodima.

Hatua hizi zinakuja baada ya Shirika la AFNET kwa kushirikiana na Ofisi ya TAKUKURU wilayani Chemba na Kamati ya Ufuatiliaji ngazi ya jamii, kuendesha zoezi la kubaini miradi ya kufuatilia katika vijiji vya Kelema Kuu na Sori mwezi Agosti mwaka huu.

Na Seleman Kodima.
Katika juhudi za kuimarisha uwajibikaji kwenye miradi ya maendeleo iliyoibuliwa na wananchi, Maafisa Watendaji wa Vijiji (VEO) na Wenyeviti wa Vijiji katika kata ya Paranga, wilayani Chemba mkoani Dodoma wametakiwa kuhakikisha wanawasilisha taarifa za mapato na matumizi kwa wananchi kwa mujibu wa sheria.

Agizo hilo limetolewa na Hilary Hilary, Mkuu wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, wakati wa kikao cha utetezi ngazi ya wilaya kupitia mradi wa Ninawajibika, unaotekelezwa na Shirika la AFNET kwa kushirikiana na taasisi ya Wajibu Institute.

Katika kikao hicho, Hilary amewakumbusha viongozi hao wajibu wao kwa wananchi, akisisitiza umuhimu wa kutoa risiti kwa kila fedha inayokusanywa kwa ajili ya miradi ya kijamii. Alisema hatua hiyo itasaidia kuondoa sintofahamu na kuimarisha imani ya wananchi kwa viongozi wao.

Akijibu changamoto zilizobainishwa kupitia mradi wa ujenzi wa zahanati na ofisi ya kijiji katika vijiji vya Sori na Kelema Kuu, Hilary amesema baadhi ya Changamoto hizo zinabebwa na wajibu wa Viongozi wa serikali za kijiji katika kuhakikisha wanatoa taarifa za miradi ya maendeleo katika mikutano ya hadhara,kujua takwimu za kaya zilizopo kwenye kijiji jukumu ambalo lipo chini Mtendaji wa kijiji,Hivyo amewaagizi watendaji hao kushughulikia changamoto hizo ambapo tayari Mtendaji wa kata ya Paranga amesema wameanza kuzifanyia kazi.

Sauti ya Hilary Hilary.
Picha ni kikao cha utetezi ngazi ya wilaya kupitia mradi wa Ninawajibika, unaotekelezwa na Shirika la AFNET kwa kushirikiana na taasisi ya Wajibu Institute.Picha na Seleman Kodima.

Awali, Katibu wa Kamati ya Ninawajibika kutoka kijiji cha Kelema Kuu, Gabriel Peter, aliwasilisha ripoti ya uchambuzi wa miradi hiyo, akitoa mapendekezo ikiwemo viongozi wa serikali ya kijiji kuwajibika kufuatilia wananchi ambao hawajatoa michango ya ujenzi.

Sauti ya Gabriel Peter.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la AFNET, Bi. Joy Njelengo, alisema lengo la mradi huo ni kuhakikisha rasilimali za umma zinadhibitiwa kwa ufanisi ili kuwanufaisha wananchi wote na kupunguza umaskini nchini.

Sauti ya Bi. Joy Njelengo

Katika hatua nyingine, Hilary aliwataka Watendaji wa kijiji cha Sori kuitisha mkutano wa kijiji ili kuwasilisha nyaraka na risiti zote za ukusanyaji wa fedha kwa ajili ya mradi wa zahanati, kama ishara ya dhana ya uwajibikaji.