Dodoma FM

INEC yawarejesha wagombea ubunge wanne

1 September 2025, 5:34 pm

Mkurugenzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Ramadhani Kailima. Picha na INEC.

Uamuzi huu ni sehemu ya kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa uwazi, haki na kwa mujibu wa sheria za nchi.

Na Mariam Kasawa.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeendelea na mchakato wa rufaa za wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani, ambapo katika kikao chake maalum kilichofanyika Agost 31, imefanya maamuzi muhimu yanayogusa mustakabali wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima, Jijini Dodoma, imeeleza kuwa Tume imekubali jumla ya rufaa nne na kutupilia mbali rufaa tisa za wagombea waliokuwa wamewasilisha malalamiko yao dhidi ya maamuzi ya wasimamizi wa uchaguzi.

Tume imezikubali rufaa mbili za ubunge na mbili za udiwani, huku ikikataa rufaa sita za ubunge na tatu za udiwani.

Ameeleza kuwa kwa upande wa ubunge, waliopata ushindi wa rufaa ni Ezekiel Gabriel Katabi, mgombea wa Chama cha CHAUMMA Jimbo la Muhambwe, pamoja na Athuman Issah Henku wa CUF Jimbo la Ikungi Mashariki. Hatua hiyo inamaanisha kuwa wagombea hao sasa wanaendelea rasmi na harakati za kampeni katika majimbo yao.

Aidha, amesema kuwa wagombea sita wa Ubunge ambao rufaa zao zimekataliwa ni Msowoya Gelard Goodluck mgombea ubunge Jimbo la Kilombero kupitia Chama cha ACT- WAZALENDO dhidi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kilombero;

Ndugu Innocent Gabriel Siriwa mgombea ubunge Jimbo la Kibamba kupitia Chama cha ADC dhidi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kibamba; David January Mhanga mgombea ubunge Jimbo la Mkuranga kupitia Chama cha CHAUMMA dhidi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mkuranga; Christina Gasper Mbise mgombea ubunge Jimbo la Ubungo kupitia Chama cha ADC dhidi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ubungo.

Kwa upande wa udiwani, ameeleza kuwa INEC imekubali rufaa mbili na kukataa tatu.