Wanafunzi 119 Mkoka wakabiliwa na upungufu wa viti mwendo
24 January 2025, 12:30 pm
Dkt. Omary Nkullo ameahidi kuzichukua changamoto zote na kuzifanyia kazi ikiwemo kuona namna ya kuwaajiri walimu wanaojitolea kuwafundisha wanafunzi wenye ulemavu katika kituo hicho.
Na Mariam Kasawa.
Wanafunzi 119 wenye mahitaji maalum waliopo katika kituo kilichopo Shule ya Msingi Mkoka wilayani Kongwa mkoani Dodoma wanakabiliwa na ukosefu wa vitimwendo.
Hayo yamesemwa na Bwana Furaha Mwashilingi, Mkuu wa kituo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mheshimiwa Mayeka Simon Mayeka alipotembelea kituo hicho kujua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Baadhi ya changamoto zilizotajwa ni Pamoja na ukosefu wa vitimwendo (wheelchairs) pamoja na changamoto za upungufu wa madarasa, walimu, wahudumu wa kuwalea watoto, miundombinu ya vyoo pamoja na ufinyu wa bajeti ya kuendeshea kituo hicho.
Kwa upande wake Mhe. Mayeka ameahidi kuendelea kushirikisha Serikali, marafiki na na wadau mbalimbali wa maendeleo ya watoto ili kusaidia kutatua changamoto zinazokabili kituo hicho na kueleza ufahamu wake wa changamoto za kulea watoto wenye mahitaji maalum na kuongeza kuwa kazi hiyo inahitaji moyo wa kipekee pamoja na ukarimu.
Aidha Mhe Mayeka amewasisitiza walimu na walezi wa wanafunzi hao kusimamia usafi wa mazingira na ulinzi na usalama kwani uharibifu mara nyingi hutokea kwenye udhaifu wa ulinzi na malezi mabovu.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dkt. Omary Nkullo ameahidi kuzichukua changamoto zote na kuzifanyia kazi ikiwemo kuona namna ya kuwaajiri walimu wanaojitolea kuwafundisha wanafunzi wenye ulemavu katika kituo hicho.