Dodoma FM

Serikali yatangaza rasmi uchaguzi wa serikali za mitaa

15 August 2024, 5:29 pm

Picha na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati akitangaza Tangazo la uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 jijini Dodoma.Picha na George John.

Uchaguzi wa mwisho wa Serikali za Mitaa ulifanyika mwezi Novemba mwaka 2019, hivyo, uchaguzi mwingine unatakiwa kufanyika Novemba, 2024.

Na Seleman Kodima.
Serikali imetangaza kuwa terehe 27 Novemba mwaka huu uchaguzi wa serikali za mitaa utafanyika Tanzania Bara.

Tangazo hilo limetolewa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati akitangaza tangazo la uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 jijini Dodoma.

Waziri Mchengerwa amewataka wananchi kujitokeza tarehe hiyo kupiga kura, kugombea na kuwania nafasi mbalimbali huku akitoa msisitizo suala kufanya kampeni kwa amani .

Sauti ya Mhe. Mohamed Mchengerwa.

Akizungumzia utoaji wa elimu ya mpiga kura ,Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema zoezi hilo litaanza Agosti 16 na kumtaka Mkurugenzi wa Tamisemi anayeshughulia suala hilo kuanza kufanyia kazi ili watanzania wapate elimu.

Sauti ya Mhe. Mohamed Mchengerwa.
Picha mwenyenyekiti wa wakuu wa mikoa Tanzania bara Mh. Martin Shigela .Picha na George John.

Uchaguzi wa mwisho wa Serikali za Mitaa ulifanyika mwezi Novemba mwaka 2019, hivyo, uchaguzi mwingine unatakiwa kufanyika Novemba, 2024. Uchaguzi huu unaongozwa na Kanuni za Uchaguzi wa Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ngazi ya vijiji, Vitongoji na mitaa katika Mamlaka za Wilaya na Mamlaka za Miji, Matangazo ya Serikali Na. 571, 572 573 na 574 ya Mwaka 2024.

Ikumbukwe kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara 145 na 146 inaelezea uwepo wa Serikali za Mitaa pamoja na madhumuni yake. Mojawapo ya madhumuni ya kuwepo kwa Serikali za Mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi na Kauli mbiu ya mwaka huu ya Uchaguzi wa Serikali za mitaa inasema “SERIKALI ZA MITAA, SAUTI YA WANAINCHI, JITOKEZE KUSHIRIKI UCHAGUZI.