Wazazi wazua taharuki taarifa za kutekwa kwa mtoto
14 August 2024, 4:48 pm
Dodoma TV Inaendelea kufatilia tukio hili kwa ukaribu ili kujua ukweli kuhusu madai ya Mtoto kutekwa na Watu wasiojulikana ambao kulingana na maelezo ya Watoto wenzake wanasema mwenzao aliitwa na Watu waliokuwa kwenye Gari na kumchukua kisha kuondoka nae.
Na Fred Cheti.
Wazazi wa Watoto wanaosoma katika Shule ya Msingi Jitegemee iliyopo Kata ya Ndachi Jijini Dodoma wamevamia Shule hiyo baada ya uwepo wa taarifa ya Mtoto kutekwa katika maeoneo ya Shule hiyo.
Dodoma TV imefika katika eneo hilo na kukuta hali ya taharuki ambayo iliwalazimu Polisi kufika shuleni hapo na kuwatuliza Wazazi hao ambao inasemekana walifika kwa lengo la kuangalia usalama wa Watoto wao.
Mwalimu Onesphory Massawe ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Jitegemee hapa anaeleza tukio la Wazazi kufika shuleni hapo lilivyokua huku akikanusha kuwa Mtoto anaedaiwa kutekwa na Watu wasiojulikana si Mwanafunzi wa Shule hiyo.
Mmoja wa Wanafunzi ambae anasoma katika Shule hiyo amesema amewahi kunusurika kutekwa na Watu asiowafahamu wakati akienda Shule majira ya saa 2 asubuhi na ameeleza hali ilivyokuwa licha ya kufanikiwa kuwakimbia Watu hao.
Wakati haya yakijiri ni siku moja imepita tangu Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma SACP Anania Amo kukanusha taarifa za uwepo wa tukio lolote la Mtoto kutekwa na kuwataka Wananchi kuacha kuzua taharuki kwa kutoa taarifa wasizokuwa na uhakika nazo.