Programu ya makuzi, malezi na maendeleo ya awali ya mtoto yatakiwa kusimamiwa bila mkwamo
15 December 2023, 7:40 am
Mafanikio ya utekelezaji wa programu hiyo kwa takribani miaka 2 tangu uzinduliwe mwaka 2021 hayakuletwa na Serikali pekee.
Na Mariam Kasawa.
Watekelezaji wa programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto wametakiwa kwenda kusimamia ipasavyo mipango waliyojiwekea iweze kutekelezeka bila mkwamo wowote.
Rai hiyo imetolewa na Naibu katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju alipo kuwa akifunga Mkutano wa Kitaifa wa Wadau Watekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) jijini Dodoma.
Amesema mafanikio ya utekelezaji wa programu hiyo kwa takribani miaka 2 tangu uzinduliwe mwaka 2021 hayakuletwa na Serikali, Serikali ni sehemu tu na watu waliofanikisha utekelezwaji kwa kiasi kikubwa ni wadau ambao ni Children in Crossfire,UTPC na TECDEN.
Naye Mkurugenzi wa idara ya afya, ustawi wa jamii na lishe kutoka TAMISEMI Bw.Rashid Mfaume amesema katika majadiliano waliyoyafanya kwenye Mkutano huo, azimio la pili wamekubaliana ya kwamba ifikapo mwezi April 2024, Waratibu,mashirika yasiyo ya kiserikali(NG’Os),na Serikali ngazi ya mikoa na halmashauri watahakikisha kwamba kupitia programu hiyo watakuwa wamefikia halmashauri nyingine chache zilizobaki nchini .
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Children in Crossfire Bw.Craig Ferla amewaasa watekelezaji wa programu hiyo kuzidisha malezi bora kwa watoto ili kuweza kujenga taifa bora la kesho.