Wananchi pigeni vita usafirishaji haramu wa binadamu
13 November 2023, 7:03 pm
Biashara hiyo imekuwa ikisababisha athari ikiwemo kutumikishwa kwa ujira mdogo na wengine kutolewa baadhi ya viungo bila ridhaa huku utumikishwaji wa majumbani ukitajwa kuwa moja ya mambo yanayowaathiri wasichana wengi.
Na Bernad Magawa.
Jamii imetakiwa kupiga vita suala la usafirishaji haramu wa binadamu, biashara ambayo imeelezwa kuendelea kushamiri duniani kote na kusababisha madhara makubwa kwa wahanga.
Akizungumza katika mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi mbali mbali wilayani Bahi wakiwemo viongozi wa dini, waratibu elimu na watendaji kata pamoja na idara za Polisi, Mahakama, uhamiaji, ustawi wa jamii pamoja na wengine yaliyofanyika katika ukumbi wa kanisa katoliki Bahi, Mratibu wa mafunzo hayo yanayotolewa na Umoja wa Masista wakatoliki Tanzania (TCAS) Sr. Jansi Jai Stanslaus alisema kwa mujibu wa takwimu za shirika la kazi Duniani (ILO) za mwaka 2021 watu milioni 49.6 walikuwa utumwani mwaka huo.
Naye Paroko wa Parokia y Bahi Padri Levocatus Majuto akizungumza katika mafunzo hayo amewashauri vijana kujishughulisha na kazi mbalimbali za kujipatia kipato halali na kuachana na maisha ya mteremko huku akisisitiza serikali kuwawezesha vijana mitaji ili wajiajiri.
Katika mafunzo hayo, afisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Bahi Liberata Sunday alieleza ukubwa wa biashara ya usafirishaji haramu wa binadamu wilayani humo huku kijiji cha Chimendeli kata ya Chikola kikitajwa kuwa kinara katika biashara hiyo na kuiomba jamii kuungana kwa pamoja katika kutokomeza suala hilo.
Awali, mkufunzi wa mafunzo hayo Bwana Christopher Mavunde alieleza maeneo mengi wanayopelekwa kufanya kazi watu wanaosafirishwa kupitia biashara haramu huku biashara ya viungo vya binadamu ikihusishwa.