Ubakaji, ulawiti kwa watoto wakithiri Dodoma
13 November 2023, 4:31 pm
Ripoti hiyo ni kwa mujibu wa Kituo cha One stop center kwa mwezi Septemba 2023 ambapo takwimu zimebainisha kuwa mkoa wa Dodoma matukio ya ukatili wa kijinsia kwa watoto 130 kwa matukio ya ubakaji huku watoto 69 wakilawitiwa.
Na Seleman Kodima.
Inaelezwa kuwa wastani wa watoto sita hadi saba kwa wiki wanafanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono hasa ubakaji na ulawiti.
Hayo yamesemwa na Afisa Ustawi mkoa wa Dodoma Josephine Mwaipopo, wakati akizungumza na wazazi na walezi katika mahafali ya Pre- Unit shule ya Morning Stars ambapo amesema hali ya ukatili kwa mwezi wa tisa inatoa tafsiri ya matukio ya ukatili wa kijinsia kwa watoto kuongezeaka.
Amesema watoto wanaothirika zaidi katika ripoti hiyo ni kundi lenye umri wa miaka mitano hadi tisa ambapo walifanyiwa ukatili wa kingono kwa kulawitiwa wakiwa ni wakiume .
Amesema umri huo umekuwa na takwimu kubwa ambapo watoto 77 walifanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia huku watoto wa kuanzia umri wa miaka kumi hadi kumi na nne, watoto 24 walibakwa huku wa kiume 22 wakilawitiwa.
Akizungumzia wanaohusika na vitendo hivyo kwa mujibu wa ripoti hiyo amesema asilimia 40 ni ndugu familia za watoto hao huku wengine wakifanyiwa ukatili huo na watu wa karibu na familia zao.