Wanafunzi watakiwa kutofumbia macho vitendo vya rushwa
13 November 2023, 4:07 pm
Na Seleman Kodima.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Alhaji Jabiri Shekimweri amewataka wanafunzi wa Shule za Sekondari Dodoma kupinga, kuchukia na kutofumbia matendo ya rushwa.
Rai hiyo ameitoa wakati akizungumza na shule 12 ambazo ziliingia fainali katika shindano la Mdahalo wa Shule za Sekondari Dodoma lililoandaliwa kwa ushirikiano wa mkuu wa wilaya ya Dodoma na Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa mkoa wa Dodoma lengo likiwa ni kuwajengea wanafunzi uwezo na ari ya kujiamini na kupambana na vitendo vya rushwa, kujieleza, kujenga hoja, kuhoji na zaidi kuwajengea uwezo wa maarifa na kitaaluma.
Alhaji Shekimweri amewaasa wanafunzi hao kuhakikisha wanakataa aina yeyote ya Vitendo vya Rushwa .
Aidha amewataka wanafunzi hao kuwa mstari wa Mbele kutoa Elimu kwa wazazi na walezi wao kuhusu Rushwa na kuwa mstari wa mbele kuhamasisha jamii kupinga Vitendo hivyo .
Mkuu huyo wa wilaya amesema amepokea mapendekezo ya ushirikishwaji wa wanafunzi wa shule za Msingi katika mashindano hayo ili kuweze kutoa nafasi ya wanafunzi wote kujengewa uwezo wa mapambano dhidi ya Rushwa.
Awali akisoma Risala kuhusu Mshindano hayo ,Mjumbe wa Sekretarieti ya mashindano hayo Mwl Salim Dewji amesema kuwa kupitia mashindano hayo wamefanikiwa kufikisha Elimu ya kupinga vitendo vya Rushwa kwa wanafunzi laki moja .
Kwa upande wake Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa mkoa wa Dodoma Amewataka washirikishi wa mdahalo huo kutambua wajibu wao wa kupambana na rushwa katika utoaji wa taarifa kwa Mamlaka zinazoshughulikia jinai.
Huu ni Mwaka wa Pili tangu kuanzishwa kwa Mashindano hayo ambayo muasisi wake ni Mkuu wa wilaya ya Dodoma ambapo Mwaka huu mashindano hayo yamehusisha shule 60 za Sekondari Dodoma na Kushuhudia shule ya Sekondari Bunge wasichana wakiwa mabingwa kwa mwaka 2023 na kuzawadia Compture mpakato na Kiasi cha Shilingi laki moja Taslimu.