Bahi Sokoni waanza utaratibu wa kusoma mapato na matumizi
30 October 2023, 2:09 pm
kupitia mkutano huo elimu mbalimbali zilitolewa ikiwemo suala la ukatili wa kijinsia.
Na. Bernad Magawa.
Kijiji cha Bahi Sokoni wilayani Bahi kimeanza kutekeleza kwa vitendo agizo la Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Bahi Zaina Mlawa alilolitoa hivi karibuni akiwaagiza viongozi wa vijiji kuhakikisha wanawasomea wananchi mapato na matumizi kupitia mikutano ya hadhara.
Ni Sauti ya Gaspar Masinjisa, Afisa Mtendaji wa kijiji cha Bahi Sokoni chenye wakazi zaidi ya elfu 14 akisoma taarifa ya mapato na matumizi ya kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/2024 kuanzia Mwezi Julai had Septemba kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Oktoba 26 na kusema kuwa katika kipindi hicho zaidi ya shilingi Millioni 10 zilikusanywa kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato.
Aidha kupitia mkutano huo elimu mbalimbali zilitolewa ikiwemo suala la ukatili wa kijinsia ambapo Mwenyekiti wa Wazee wilaya ya Bahi Dominiki Emiliani alitoa elimu hiyo kwa wananchi kama sehemu ya kuwajengea uwezo kuhusiana jambo hili.
Nao baadhi ya wananchi walipata nafasi ya kujadili taarifa hiyo, wakipongeza na kuuliza maswali mbalimbali huku Diwani wa kata ya Bahi Mheshimiwa Agostino Ndonuu akiwapongeza wananchi kwa kushiriki kikamilifu kwenye miradi ya maendeleo.
Awali akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa kijiji cha Bahi Sokoni Mh. Sifael Abel Mbeti aliwashukuru wananchi wa kijiji hicho kwa kuhudhuria huku akiwaomba kuendelea kushiriki katika shughuli zote za maendeleo kijijini hapo.