Wananchi Dodoma waomba elimu uzalishaji umeme wa jua
16 October 2023, 4:40 pm
Na Alfred Bulahya.
Wananchi Mkoani Dodoma wameiomba serikali na wadau wa masuala ya kilimo nchini kuanza kutoa elimu ya namna ya kutumia teknolojia zinazozalisha umeme wa jua ili kuongeza tija zaidi katika kilimo cha umwagiliaji.
Wananchi hao wametoa maombi hayo mapema leo wakati wakizungumza na Dodoma fm radio kwa nyakati tofauti.
Denis Jackson na Winfrida Richard ni miongoni mwa wananchi hao wanasema kwa sasa jamii imekuwa ikishindwa kukiendeleza kilimo cha umwagiliaji kutokana na kukosa elimu sahihi ya utumiaji wa miundombinu ya Sola inayozalisha umeme kupitia jua.
“wakulima wengi katika kipindi hiki wanajitahidi sana kulima kilimo hiki cha umwagiliaji lakini shida inakuja watu wanakata tamaa kwa sababu hawana elimu ya namna gani wanaweza kupata umeme kupitia jua na wakautumia umeme huo kuvuta maji kutoka kwenye vyanzo mbalimbali.
Mimi naomba serikali na wadau wengine wa sekta ya kilimo wajitahidi sana kuwekeza kwenye elimu kwa sababu elimu ndio itawasaidia wakulima kujua nini cha kufanya ili kupata huo umeme jua maana baadhi yetu tumekuwa tukiusikia tu kwenye vyombo vya habari”, alisema Jackson.
Naye Winfrida Richard alisema “unajua kuna maeneo yana vyanzo vya maji ambavyo wakulima wanaweza kuvitumia katika kilimo hiki cha umwagiliaji na wakazalisha mazao mengi tu sema shida baadhi ya watu hasa vijijini hawajui wafanye nini ili kuyavuna hayo maji na wakayatumia kuzalisha mazao.
Tunajua serikali ina mambo mengi ila sasa wakishirikiana na wadau ambao wanafanya miradi ya kilimo kwenye maeneo mbalimbali inaweza kusaidia kwa kuwa kuna mashirika huwa tunaona yanajitangaza kuuza sola na pampu za maji ambazo hizo sola zinaweza kutumika kuvuta maji yakafika kwenye hayo maeneo ambayo hayana maji na watu wakaendelea na kilimo kama kawaida”,alimaliza.
Tilizungumza na Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Agriculture Nutrition Empowerment (ANUE) bwana Mengo Chikome kufahamu wao kama wadau wanafanya nini kuhakikisha jamii inatoka kwenye kusubiri mvua za msumi hadi msimu ambapo hapa anaeleza.
“ni kweli kuna changamoto ya watu kutojua namna gani wanaweza kutumia umeme jua kuvuta maji hasa kwa wale ambao umeme haujafika kwenye maeneo yao.
Sisi kama shirika kwa sasa tumeanza kuwapatia mafunzo mbalimbali wakulima ya namna ya kutumia na kufunga sola kwenye mashamba yao ili kusaidia kuvuta maji na kupeleka kwenye mashamba yao na mafunzo hayo tumanza kwa kuwapeleka wakulima kadhaa Jijini Arusha ambako ndio tnafanyai mafunzo hayo,”. Alisema
Katika hatua nyingine bwana Mengo Chikome alitumia fursa hiyo kuwataka wakulima mkoani hapa kuanza kuchukua hatua sasa ya kuzungumza na wataalamu wa kilimo kama maafisa ugani wa kata ndani ya kata zao ili kuona namna gani watapata elimu hiyo ili kutoka katika kilimo cha mazoea na kulima kilimo chenye tija.