Wadau wa tasnia ya Maziwa Nchini watakiwa kupunguza bei ya maziwa
28 September 2023, 2:47 pm
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewaomba wadau wa tasnia ya maziwa nchini kupunguza bei ya maziwa ya Shs 1800 kwa nusu lita ili Mpango wa Unywaji Maziwa kwa watoto wote shuleni ufikie malengo.
Kauli hiyo imetolewa jana kwenye viwanja vya Furahisha Mkoani Mwanza na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni Duniani ambapo Kitaifa imefanyika Mkoani humo.
Mhe. Mnyeti amesema Serikali imefuta tozo zote zinazohusu maziwa hivyo mamlaka husika ziangalie bei muafaka eneo la vifungashio ili wadau wa Tasnia hiyo wasiingie gharama kubwa.
Amesema itakuwa ni kazi bure kuendelea kuhimiza unywaji wa maziwa kila ifikapo kilele cha maadhimisho hayo wakati uwezo wa kumudu gharama hiyo haupo kutoka kwa wazazi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi ameishukuru Wizara kwa kuona umuhimu wa maadhimisho hayo kufanyika Mkoani humo kutokana na miradi mingi ya kuboresha mifugo inatekelezwa kuanzia Shamba la Taifa la Mifugo Mabuki na kwenye baadhi ya wilaya.