Taasisi za umma zaombwa kuitumia mamlaka ya serikali mtandao
18 September 2023, 5:43 pm
Mamlaka ya serikali mtandao inatekereza program ya kukuza bunifu katika tehama kwa wanafunzi wa Elimu ya juu kuanzia kwa miaka 5 sasa tangu mwaka 2019 hadi mwaka 2023.
Na Mariam Matundu.
Taasisi za Umma zimeombwa kuitumia Taasisi ya mamlaka ya serikali mtandao katika kujenga mifumo mbalimbali ya Tehama ili kuokoa fedha nyingi zinazotumika kununua mifumo nje ya nchi .
Waziri wa ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi wa Umma na utawala bora Mh George Simbachawene ametoa rai hiyo mara baada ya kutembelea kituo cha cha ubunifu na utafiti cha mamlaka ya serikali mtandao hii leo .
Amesema Ili kuhakikisha Tehama inatoa matokeo tarajiwa kwa Uchumi wa nchi ya Tanzania jitihada mbalimbali zimefanyika ikiwemo za kisera ,kanuni , miongozo na viwango vya serikali mtandao ambavyo vimesaidia katika kusanifu ,kutengeneza na kusanikisha mifumo na miundombinu ya serikali mtandao katika taasisi za umma .
Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya serikali mtandao Eng Benedict Ndoma amesema kuwa kituo kimekuwa kikifanya tafiti katika maeneo yote ya tehama kwani tafiti hizo na bunifu zinaiweka nchi katika nafasi nzuri ya kushindana kwenye Uchumi wa kidijitali na mataifa mengine.
Nao wanafunzi wanaopata mafunzo kwa vitendo katika kituo hicho licha ya kushukuru kwa kupata fursa hiyo wameiomba serikali kuharakaisha ujenzi wa kituo kikubwa ili kuendana na Kasi ya mabadiliko ya teknolojia .