Dodoma FM

Usawa kijinsia sio kukandamiza kundi fulani

16 August 2023, 1:53 pm

Kikao kazi hicho cha siku moja, kinapokea taarifa za utekelezaji wa sekta na wadau kuhusu usawa wa kijinsia kwa kipindi Januari hadi Juni, 2023.

Na WMJJWM,  Dodoma

Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt John Jingu, amesema dhana ya usawa wa kijinsia sio kukandamiza jinsi yoyote bali kuweka mifumo mizuri itakayosaidia kuwa na fursa sawa kwa jinsi zote katika nyanja mbalimbali.

Katibu Mkuu Dkt. Jingu ametoa kauli hiyo wakati akifungua Kikaokazi kilicho wakutanisha Maafisa wa Madawati ya Kijinsia kutoka Wizara za Kisekta pamoja na Wadau wa Maendeleo walipokutana jijini Dodoma Agosti 15, 2023.

Amesema baadhi ya watu hawaelewi dhana usawa wa kijinsia, wengine wanahusisha usawa na kijinsia  na ubaguzi au kulinda kundi moja ndani ya jamii dhana ambayo sio kweli.

Aidha Dkt. Jingu amewataka Maafisa  hao kutoka Wizara za kisekta kuwa chachu ya kuwabadilisha watu walio wengi wanaodhani usawa wa kijinsia ni kuikandamiza jinsi Moja ili waweze kuelewa dhana hiyo maana yake na inavyosaidia kuleta maendeleo jumuishi katika jamii.

Dkt. Jingu ameongeza kuwa Maafisa wa  Madawati hayo wasingoje kuwasilisha taarifa pekee kama ilivyo sasa badala yake waongeze ubunifu ili shughuli wanazofanya ziweze kufahamika lakini pia kuwa na mashiko hasa kutoa elimu sahihi kuhusu usawa wa kijinsia wakianza katika ofisi zao na kwa jamii.

“Ukiwasha taa na kuiweka chini ya uvungu huwezi kupata nuru, lakini ukiweka juu nuru itaonekana hivyo hivyo katika majukumu yenu lazima mzingatie hili” amesema Dkt. Jingu

Maafisa wa Madawati ya Kijinsia kutoka Wizara za Kisekta pamoja na Wadau wa Maendeleo wakiwa katika kikao kazi hicho. Picha na WMJJWM.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Jinsia kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Badru Abdunur amesema kuwa vikao vya wataalam hao hukutana kila robo mwaka kwa lengo la kupokea taarifa za masuala ya jinsia na kuweka mikakati ya kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao hivyo katika kikao hicho watajadiliana zaidi kuwa na mbinu bunifu katika kuhakikisha dhana ya usawa wa kijinsia inaeleweka kwa jamii.

Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt John Jingu akizungumza katika kikao kazi hicho. Picha na WMJJWM.

Kwa Upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa UN Women kwenye mkutano huo, Usu Malya ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa hatua inayopiga katika kushughulikia masuala ya jinsia hasa katika kuhakikisha inaratibu madawati ya jinsia katika Wizara za kisekta ili kuweka nguvu katika kuhakikisha masuala ya kijinsia yanazingatiwa hasa katika upangaji wa mipango na bajeti mbalimbali za maendeleo.