TMDA yaanzisha mfumo wa ufuatiliaji wa usalama wa dawa
10 August 2023, 1:37 pm
Pamoja na hayo TMDA imesisitiza Wagonjwa na jamii kutoa taarifa mapema kwenye hospitali ,kituo cha afya,zahanati au duka la dawa ambapo matibabu yalitolewa ambapo utoaji wa taarifa za madhara ya dawa ni jukumu la kila mmoja ili kusaidia kuboresha sekta ya afya.
Na Selemani Kodima .
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba TMDA kanda ya Kati imesema mamlaka hiyo imeanzisha mfumo wa Ufuatiliaji wa Usalama wa Dawa ambapo mfumo huo unajumuisha utambuzi ,tathimini ,uelewa na udhibiti wa madhara yatokanayo na matumizi ya Dawa.
Pia imesema mfumo huo Unalenga katika kuhakikisha kuwa matibabu yaliyosahihi yanatolewa kwa wagonjwa na Unawezesha kufahamu madhara pamoja na sababu inazosababisha madhara baada ya dawa kusajiliwa na kuanza kutumika.
Hayo yamesemwa na Mtaalamu kutoka TMDA kanda ya kati Bi,Seraphina Cleophace wakati akizungumza na Taswira ya Habari kuhusu TMDA wanafuatilia kwa namna gani Madhara yatokanayo na Matumizi ya Dawa,ambapo ametoa ufafanuzi wa namna Mamlaka hiyo inavyodhibiti madhara ya dawa .
Kwa Upande wake Meneja wa TMDA Kanda ya kati Bi,Sonia Mkumbwa ametoa wito kwa wananchi pamoja na wataalamu wa afya kutoa taarifa za madhara ya Dawa kwa wakati ili kurahisisha udhibiti wa ubora ,usalama na ufanisi wa dawa huku lengo ni kulinda afya ya Jamii.
Kwa upande Mwingine TMDA wamesema zipo hatua ambazo wanachukua baada ya kufanya tathimini ya madhara ya dawa ikiwa ni pamoja na kuagiza watengenezaji wa dawa kuanisha madhara yaliyojitokeza kwenye vikaratasi ambatanishi vya dawa zao .