Dodoma FM

Mashujaa kuadhimishwa kwa mara ya kwanza mji wa kiserikali Mtumba

20 July 2023, 4:18 pm

Mkuu wa mkoa wa Dodoma Mh. Rosemary Senyamule akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho hayo . Picha na Mariam Kasawa.

Mkuu wa mkoa wa Dodoma amesema maadhimisho hayo yamekamilika kwa asilimia 100 ambapo amesisitiza wananchi kujitokeza kwa  wingi kwa ajili ya kuadhimisha siku hii muhimu ambayo inafanyika kwa mara ya kwanza katika kiwanja kipya kilichopo eneo la Mtumba.

Na Mariam Kasawa.

Kuelekea maadhimisho ya siku ya Mashujaa Mkoani Dodoma , Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo yatakayofanyika katika uwanja mpya wa Mashujaa uliopo mji wa serikali Mtumba.

Akitangaza maandalizi ya kuelekea siku hiyo mkuu wa mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu yatafanyika katika uwanja mpya wa kudumu wa Mashujaa uliopo mji serikali tofauti na hapo awali katika viwanja vya Jamatin vinavyopatikana mjini Dodoma.

Mhe Senyamule amesema kuwa shughuli za Mashujaa zitatanguliwa na uwashaji wa Mwenge wa Mashujaa saa 6:00 Usiku wa tarehe 24 Julai, 2023 kuamkia tarehe 25 Julai 2023 

Sauti ya Mkuu wa Mkoa.
Picha ni Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa katika mkutano huo. Picha na Mariam Kasawa.

Aidha mkuu wa mkoa wa Dodoma amepata heshima ya kuuwasha Mwenge huo wa Mashujaa kwa niaba ya wakazi wa Dodoma huku  Mwenge huo ukitegemewa kuzimwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma 25 Julai 2023 saa 6:00 Usiku.

Mhe Senyamule amempongeza Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuibua wazo na kutoa maelekezo ya kutafuta eneo kubwa la kudumu kwa ajili ya kuadhimisha kumbukumbu ya siku ya mashujaa.