Kilimo cha umwagiliaji chachu uhakika wa chakula
27 June 2023, 4:38 pm
Mwema ametumia nafasi hiyo kuwahamasisha wananchi kujiingiza kwenye kilimo cha umwagiliaji ili kusaidia upatikanaji wa chakula kwa wingi na kwa uhakika.
Na Bernadetha Mwakilabi.
Mwakilishi wa shirika la chakula duniani (WFP) nchini Tanzania Bi Sarah Gordon- Gibson amesema kuwa kilimo cha umwagiliaji ni chachu itakayosaidia uhakika wa upatikanaji wa chakula kwa jamii.
Gibson ameyasema hayo alipotembelea wilayani Kongwa kujionea hali inayoendelea changamoto na namna ya kuzitatua ili zisijirudie awamu nyingine katika skimu ya umwagiliaji iliyopo Tubugwe wilayani humo ili kukuza maendeleo ya soko la kilimo.
Pia Gibson ameongeza kuwa kutokana na kukua kwa kilimo cha umwagiliaji kuna haja ya kwenda kukagua soko la mazao la kimataifa la Kibaigwa kwani wanahitaji kupata soko zuri na kubwa kwaajili ya kununua mahindi na mtama kutoka Tanzania.
Kwa upande wake Afisa kilimo wilaya Kongwa Bwana Shija ameshukuru shirika la chakula duniani WFP kwa ushirikiano mkubwa na nguvu wanayoitoa kukuza miradi ya kilimo wilayani humo.
Akiongea kwa niaba ya wilaya mkuu wa wilaya Kongwa Mheshimiwa Remidius Mwema Emmanuel ametaja changamoto zinazokabili skimu ya umwagiliaji ya Tubugwe kuwa ni pamoja na uharibu wa mazingira unaofanywa na wananchi hali inayopelekea upungufu wa upatikanaji wa maji.
“Kilimo cha umwagiliaji ni maji kama hakuna maji hatuwezi kuendesha kilimo cha umwagiliaji watu wanajaribu kuharibu mazingira kwa kukata miti tutapata wapi maji” alisema Mwema.
Pamoja na changamoto hiyo Mwema amesema wilaya kwa kushirikiana na ofisi ya misitu (TFS) wameweza kupanda miti kuzunguka eneo la mradi, na kuwataka wananchi kulinda mazingira kuanzia ngazi ya kaya mtu mmoja mmoja.