Wanandoa watakiwa kumtegemea Mungu
26 June 2023, 3:56 pm
Tukio hilo la kufungisha ndoa liliambatana na sherehe za dekania ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji zilizofanyika parokiani Kigwe ambazo zilitanguliwa na uzinduzi wa nyumba mpya ya mapadri parokiani hapo.
Na Bernad Magawa.
Makamu wa Askofu Mkuu wa Jimbo kuu katoliki Dodoma Padri Michael Gaula ametoa rai kwa wanandoa kumtanguliza Mungu katika maisha yao ya pamoja kwa kuziombea familia zao ili waweze kudumu katika upendo na mshikamano.
Akifungisha jozi mbili za ndoa katika parokia ya Kigwe, Padri Gaula amesema ndoa ni baraka kutoka kwa Mungu ikikusudia kufanya uumbaji ambao Mungu mwenyewe aliuanzisha hivyo ni vema wanandoa kuheshimiana na kupendana ili waweze kuyaishi vema maagano yao.
Padri Gaula amesisitiza wanandoa kuwajibika kila mmoja kadiri ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu ili ndoa ziweze kustawi hatimaye kuwa na familia imara zenye kumjua mungu.
Tukio hilo la kufungisha ndoa liliambatana na sherehe za dekania ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji zilizofanyika parokiani Kigwe ambazo zilitanguliwa na uzinduzi wa nyumba mpya ya mapadri parokiani hapo iliyojengwa kwa michango ya waamini ikigharimu Shilingi milioni 76 mpaka kukamilika, huku watoto saba wakibatizwa na zaidi ya 160 kupewa sakramenti ya kipaimara.