Bahi: Adha ya maji Lamaiti yafikia tamati
7 June 2023, 5:06 pm
Mradi huo uliojengwa kwa hisani ya shirika la Water Mission ukigharimu zaidi ya milioni 800 za kitanzania, ni moja ya miradi mikubwa ya maji wilayani Bahi na umetatua changamoto za maji safi na salama kwa wananchi wa kijiji hicho cha Lamaiti.
Na Bernad Magawa.
Wananchi wa kijiji cha Lamaiti wilayani Bahi wameondokana na tatizo la kukosa maji safi baada ya mradi mkubwa wa maji kukamilika na kuanza kutoa huduma kijijini hapo.
Afisa tawala wa wilaya ya Bahi Jeremia Mapogo akizungumza baada ya kutembelea mradi huo akiambatana na kamati ya ulinzi na usalama pamoja na wakuu wa idara na taasisi mbalimbali amelipongeza shirika la Water Mission kwa kusaidia wananchi hao.
Naye kaimu mhandisi wa RUWASA wilaya ya Bahi Boniphace Bihemu ameeleza shughuli namna mradi huo ulivyotekelezwa na kuwashukuru wananchi wa kijiji cha Lamaiti kwa kujitoa nguvu kazi katika mradi huo.
Kwa upande wake Mhandisi Daudi Meda ambaye ndiye aliyesimamia mradi huo amesema mradi umekamilika na tayari wananchi wameanza kupata huduma huku katibu wa chombo cha watumiaji maji Charles Ndigwa akieleza baadhi ya changamoto zinazojitokeza na kusababisha baadhi ya vituo kutokutoa maji ipasavyo.