Wataalam wa mipango, uratibu watakiwa kutenga bajeti kutekeleza program ya MMMAM
2 June 2023, 6:45 pm
Waziri Dkt. Gwajima amesema katika bajeti zijazo itabidi uhakiki wa bajeti ufanyike ili kubaini kama bajeti ya utekelezaji wa Programu hiyo umezingatiwa.
Na Mariam Matundu.
Rai imetolewa kwa wataalam wa mipango na uratibu katika sekretarieti za mikoa kuhakikisha wanatenga bajeti za utekelezaji wa programu jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM) ili kufanikisha malengo ya uanzishwaji wa programu hiyo.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa rai hiyo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya utekelezaji wa programu hiyo kwa maafisa maendeleo ya jamii, ustawi wa jamii, makatibu tawala wasaidizi wa mipango na uratibu wa sekretarieti za mikoa na wadau jijini Dodoma Juni 1, 2023.
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii Patrick Golwike, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu, amebainisha kuwa mafunzo hayo ni mwendelezo wa jitihada za wizara na wadau kuhakikisha utekelezaji wenye ufanisi wa programu hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Children in Crossfire, Craig Ferla amesema mara nyingi kuna changamoto ya utekelezaji wa programu hasa ngazi za chini hivyo ni faraja ya pekee kuwa na makatibu tawala wasaidizi wa mipango na uratibu kwenye mafunzo haya.
Naye Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu kutoka Mkoa wa Dar es Salaam Chillah Moses ameishukuru Wizara kwa jitihada zinazofanywa kuhakikisha utengaji wa bajeti ya kutekeleza programu hiyo kwa manufaa ya watoto nchini.