Wamiliki wa nyumba za kulala wageni Bahi watakiwa kufuata taratibu na sheria
17 March 2023, 3:15 pm
Ni marufuku watu wa jinsia moja kulala kwenye chumba kimoja, badala yake sheria imeruhusu watu wawili wa jinsia tofauti kulala chumba kimoja lakini waliohalalishwa kwa mujibu wa imani yao.
Na Benard Magawa.
Mkuu wa Jeshi la Polisi wilaya ya Bahi SSP Idd Ibrahim Abdalah amewaagiza wamiliki wa nyumba za kulala wageni wilaya humo kufuata taratibu za uendeshaji wa nyumba hizo kwa mujibu wa sheria za nchi na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuendelea kulinda amani ya wilaya hiyo.
SSP Abdala amesema hayo kupitia elimu ya usalama wa raia na mali zao aliyoitoa kwa wanachi wilayani humo kwa lengo la kuwakumbusha wananchi kuendelea kuzingatia utii wa sheria bila shuruti na kuepuka vitendo vya uhalifu vinavyoweza kuvuruga amani ya wilaya hiyo.
Amesema ni marufuku watu wa jinsia moja kulala kwenye chumba kimoja, badala yake sheria imeruhusu watu wawili wa jinsia tofauti kulala chumba kimoja lakini waliohalalishwa kwa mujibu wa imani yao na kukemea vikali wamiliki wanaovunja taratibu hizo.
Aidha amesema sheria haimvumilii uhalifu wa aina yoyote katika jamii na kutoa rai kwa wazazi kuwaonya vijana wao wenye tabia ya udokozi huku akiwaasa vijana wenye tabia ya hiyo kutafuta kazi halali za kujiingizia kipato ili kuepukana na uhalifu.
Amesema vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa lakini cha ajabu vijana wengi ndio waliojaa magerezani kuliko wazee hali ambayo inazorotesha uzalishaji kwa taifa letu na kuongeza kuwa serikali haipendezwi na mwenendo huo na kuwaomba vijana kujikita katika shughuli za uzalishaji badala ya uhalifu huku akiwaomba wazazi kuwalea vijana katika maadili yanayokubalika.
Hata hivyo amewakumbusha wananchi kuhakikisha wanaripoti vitendo vyote vya uhalifu ukiwemo udokozi vinavyotokea kwenye maeneo wanayoishi na kuacha kuficha taarifa hizo ili kutokomeza kabisa vitendo hivyo.