Idara ya Elimu Msingi Bahi yazidi kung’ara
17 February 2023, 10:53 am
Na Benard Magawa
Ikiwa imetimu takribani zaidi ya miezi miwili tangu kutangazwa kwa matokeo ya darasa la saba hapa nchini Disemba mwaka 2022 ambayo yaliweka historia mpya kwa wilaya ya Bahi baada ya wilaya hiyo kuwa kinara mfululizo kwa miaka mitatu katika mkoa wa Dodoma, na kuwasha mshumaa wa mabingwa kumi bora kitaifa, huku ikiwa imeongoza miongoni mwa halmashauri za wilaya na miji hapa nchini, idara ya elimu msingi wilayani hapo imekuwa kivutio kwa wilaya nyingi hapa nchini kwenda kujifunza njia na mbinu za mafanikio.
Hayo yamejidhihirisha baada ya mfululizo wa ugeni wa timu za walimu, walimu wakuu,maafisa elimu kata na wilaya zikiwemo Dodoma Jiji, wilaya ya kongwa na Wilaya ya kondoa kufanya ziara za kujifunza kwa wenyeji Bahi ambao sasa wamekuwa wakufunzi wa mafanikio Kielimu kwa wenzao, ambapo februari 16,2023 imekuwa zamu ya Wilaya ya Mpwapwa ambao walikwenda wilayani Bahi kujifunza mambo mbalimbali.
Akieleza njia zilizowafikisha kwenye mafaikio hayo, Afisa elimu msingi wa wilaya hiyo Boniface Wilison ambaye amesifiwa kwa usimamizi madhubuti wa idara hiyo, amesema silaha pekee wanazozitumia ni kujenga molari ya kazi kwa walimu, kuaminiana kazini na kuheshimiana huku akieleza jinsi walimu wakuu wilayani humo wanavyoongoza kwa vitendo na siyo maneno.
“Pamoja hayo pia uwajibikaji ni moja ya mbinu iliyotufikisha hapa kwani kila mwalimu bila kujali cheo alicho nacho anawajibika ipasavyo, mfano mwalimu Mkuu hapa kwetu wana vipindi vingi kuliko walimu anaowasimamia, anakuwa wa kwanza kufika kazini na wa mwisho kutoka, pia tuna toa motisha kwa wanaofanya vizuri huku tukiwa na ushirikiano na viongozi wa chama na serikali.” Amesema wilison
Amesema baada ya kufanya vizuri na kuingia kumi bora kitaifa kwa sasa Bahi wameanza mkakati wa kuingia tano bora kitaifa katika matokeo ya darasa la saba mwaka 2023 huku akielezea hali ilivyokuwa hapo awali na njia walizotumia kuhakikisha wanasonga mbele.
Baada ya kupokea maelekezo ya kutosha kutoka kwa Afisa elimu na walimu wakuu wa wilaya ya Bahi, baadhi ya walimu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa wameeleza namna ziara hiyo ilivyowajengea uwezo huku wakitanabaisha namna watakavyo kwenda kuzitumia mbinu walizopewa kwaajili ya matokeo chanya.