Wananchi waiomba serikali kupitia Wizara ya Afya kutoa elimu juu ya homa ya manjano
21 March 2022, 2:06 pm
Na; Neema Shirima.
Baadhi ya wananchi Mkoani Dodoma wameiomba serikali kupitia wizara ya afya kutoa elimu juu ya ugonjwa wa homa ya manjano na namna ya kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.
Wakizungumza na taswira ya habari wananchi hao wamesema kuwa jamii bado haina uelewa juu ya ugonjwa huo lakini pia hawajui ni kwa namna gani wataweza kuchukua tahadhari.
Aidha kwa upande wake Gasper Kundael amesema yeye anaelewa kuwa ugonjwa wa homa ya manjano unaenezwa na mbu na dalili zake ni pamoja na kutapika na ngozi kuwa ya njano lakini bado hana uelewa wa namna ya kujikinga
Ameiomba serikali iweze kutoa elimu juu ya ugonjwa huo na matibabu yake lakini elimu zaidi juu ya namna ya kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa huo na pia katika suala la chanjo ya homa ya manjano
Maoni hayo yamekuja kufuatia siku kadhaa zilizopita baada ya waziri wa afya Mh Ummy Mwalimu kutangaza kuwepo kwa ugonjwa wa homa ya manjano katika nchi jirani ya Kenya.