Wakazi wa Zuzu waiomba serikali kuwalipa fedha za fidia ya maeneo yao
14 October 2021, 12:23 pm
Na; Benard Filbert.
Wakazi wa mtaa wa Zuzu jijini Dodoma wameiomba serikali kuwalipa fedha za fidia ya maeneo ambazo waliahidiwa baada ya kuondolewa katika maeneo yao kupisha kujengwa kwa miundombinu ya umeme wa reli ya kisasa (Standard Gauge).
Wametoa malalamiko hayo wakati wakizungumza na taswira ya habari ambapo wamebainisha kuwa waliondolewa katika maeno hayo toka mwaka jana na waliahidiwa kupewa fedha hizo mwezi wa pili mwaka huu lakini hawajapewa chochote huku viongozi wao wakikataa kutoa ushirikiano wa suala hilo.
Joshua Kajembe ni mwenyekiti wa mtaa wa Zuzu amesema ni kweli wananchi hawajapewa fedha zao za fidia licha ya wao kusimamia zoezi hilo hali inayosababibisha wananchi kukosa imani na viongozi hao.
Taswira ya habari imemtafuta mtendaji wa kata ya Zuzu bwana Bazir Benard amesema suala hilo halina utata wowote na wizara ya fedha imemaliza taratibu zote za kuhakiki majina ya wananchi kwa ajili ya malipo na mwezi huu mwishoni kila mwananchi atapewa fidia yake.
Wakazi wa kata ya Zuzu waliondolewa katika maeneo yao ambayo yapo karibu na sehemu ambayo mradi wa reli ya kisasa unapita tangu mwaka jana nakuahidiwa kupewa fidia kila mmoja.