Dodoma FM

Serikali yatakiwa kuongeza nguvu katika kuwekeza na kupambana na magonjwa ya Afya ya akili

12 October 2021, 12:57 pm

Na; Shani Nicolous.


Wito umetolewa kwa serikali kuongeza nguvu ya kuwekeza katika magonjwa ya afya ya akili .

Wito huo umetolewa na Rais na muasisi kutoka shirika la afya ya akili ya Jamii Tanzania (CMHI-Tanzania) Dr. Joshua John na kusema kuwa afya ya akili inahitaji pesa nyingi katika utekelezaji wake hivyo ni vyema serikali ikatambua umuhimu wa kuwekeza kwaajili ya kuongeza nguvu ya mapambano.

Amesema kuwa njia pekee ya kupambana na magonjwa ya afya ya akili ni kutoa elimu ya kutosha kwa jamii ambayo itasaidia watu kufahamu zaidi umuhimu wake pamoja na kutembelea makundi mbambali, shule , vyuo , vituo vya kulelea watoto yatima , magereza mbalimbali na sehemu nyingine ili kuufikisha ujumbe na kujua hali zao kisikolojia .

Ameongeza kuwa wadau mbalimbali wanao husika na utengenezaji wa sera kwa maana ya seriakali na wadau wake ni vyema kutumia nguvu kubwa kuongeza elimu juu ya afya ya akili na jinsi inavyoweza kuathiri uchumi wa nchi na maendeleo yake kwani nchi haiwezi kuendelea bila wananchi wenye afya bora ya akili.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi jijini hapa wamesema kuwa baada ya kilele cha maadhimisho ya afya ya akili wameona ongezeko la magonjwa ya afya ya akili hivyo serikali itafute njia mbadala kukabiliana na changamoto hiyo.

Jumuiya ya Kimataifa tarehe 10 Oktoba, 2021, iliadhimisha Siku ya Kimataifa ya Afya ya Akili, iliyokuwa na kauli mbiu isemayo “Afya ya Akili Katika Ulimwengu Usio na Usawa.” ambapo takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kwamba, hadi kufikia mwaka 2020 watu bilioni moja walikuwa wanaishi na magonjwa ya akili huku wengi walioko hatarini ni wale wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 39.