Jamii yaaswa kuacha tabia ya kuchangia nguo ili kuepuka magonjwa ya kuambukizwa
20 September 2021, 12:04 pm
Na; Alfred Bulahya.
Jamii imeshauriwa kuacha kuchangia nguo na badala yake kila mmoja atumie mavazi yake ili kuepusha kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali ya kuambukiza.
Wito huo umetolewa na Tabibu Joseph Zabron Kusanya wakati akizungumza na Taswira ya habari ofisini kwake ambapo amesema kuwa kuchangia mavazi ni moja ya njia ambayo inaweza kusambaza vijidudu, virusi na bakteria na kusababisha magonjwa.
Ameyataja mavazi ambayo yanaweza kusababisha kusambaa kwa magonjwa ni pamoja na mashuka, suruali, shati,soksi,viatu na nguo za ndani.
Aidha amesema magonjwa yanayoweza kuambukizwa kutokana na kuchangia nguo ni pamoja na magonjwa ya ngozi, fangasi ambayo hasa yanaweza kuathiri miguu,mikono, ngozi ya kichwa na sehemu mbalimbali za mwili.
Baadhi ya wananchi jijini Dodoma wameiambia taswira ya habari kuwa suala la kuchangia mavazi linatokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuzoeana baina ya watu au kikundi jinsi kinavyoishi hivyo ni jukumu la wataalamu wa afya kuanza kutoa elimu kwa jamii ili itambue madhara yake.