Serikali imesema itaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na ugonjwa wa uviko 19
2 September 2021, 1:53 pm
Na ; Fred Cheti.
Serikali imesema kuwa itaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na ugonjwa wa Uviko 19 pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma za afya katika maeneo yote Nchini ili kukabiliana na ugonjwa huo.
Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni na Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa katika kipindi cha maswali na majibu wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mh. Halima Mdee aliyeuliza kuwa Serikali ina mikakati gani ya ziada ya kupamabana na ugonjwa huo .
Aidha Mh. Majaliwa amesema kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na Mataifa mengine Duniani likiwemo pia shirika la afya Duniani kwa kuwatumia wataalamu wa afya wa ndani ya nchini katika kutafuta suluhisho la ugonjwa huo
Katika hatua nyingine Mh. Majaliwa ametoa wito kwa watanzania wote kuendelea kuchukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa huo kama wanavyoelekezwa na wataalamu wa afya na kuacha pia upotoshaji ikiwemo suala la chanjo ambayo inaendelea kutolewa Nchini.
Bunge la 12 limeendelea leo Agosti 2 Jijini Dodoma ambapo ilikuwa ni kikao cha 3 cha Bunge katika kipindi cha Maswali na Majibu na baadhi ya wabunge wamepata nafasi ya kuuliza maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri mkuu.