Wakazi wa Jiji la Dodoma waipongeza Serikali kwa kufanya marekebisho sheria ya tozo za miamala
1 September 2021, 1:06 pm
Na;Yussuph Hans.
Wakazi Mkoani Dodoma wamepongeza hatua ya Serikali kufanyia marekebisho sheria mpya ya tozo za miamala huku wakiomba serikali kuendelea kuangalia namna ya kupata fedha za kuboresha huduma za kijamii Nchini.
Wakizungumza na taswira ya habari kwa nyakati tofauti wakazi hao wamesema kuwa Serikali haina budi kuangalia vyanzo mbadala ambapo kwa sasa tozo za miamala zimekuwa msumari wa Moto kwa wananchi hususani maeneo ya Vijijini.
Mapema leo Waziri wa Fedha na Mipanga Dkt. Mwigulu Nchemba wakati akizungumza na waandishi wa habari Mkoani Dodoma amesema kuwa gharama za tozo zimepunguzwa kwa asilimia 30 huku kazi zikiwa zinaendelea.
Ameongeza kuwa Serikali imeachia miamala zaidi ya Milioni 29 kwa watu ambao wanatumiana kuanzia shilingi moja mpaka Sh999 kutokana na dira ya Rais kuto kukusanya pesa tu bali ni pamoja na kuzingatia ustawi wa jamii.
Tozo za miamala ya simu kuanzia leo Septemba Mosi zimeelekezwa kwenye sekta ya elimu (kujenga/kukarabati madarasa na madawati) ili kupanua fursa ya elimu kwa watoto wengi zaidi, huku makusanyo yaliyoishia Agost 31, 2021 zitatumika kujenga vituo vya afya 220 kwenye tarafa zote Nchini ambazo hazikuwahi kuwa na vituo vya afya tangu uhuru.