Wadau waizungumzia kumbukumbu ya biashara ya utumwa Duniani.
23 August 2021, 1:53 pm
Na; Fred Cheti.
Ikiwa leo Agosti 23 ni siku ya kumbukizi ya biashara ya utumwa Duniani bado inaelezwa kuwa athari za biashara hiyo ambayo inayotajwa kama moja ya ukatili wa kupindukia uliowahi kutokea kwa mwanadamu zinaendelea kuonekana duniani.
Hiyo ni kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa ambapo inasema kuwa bado kuna umuhimu wa Dunia kuchukua hatua zaidi ili kuzishugulikia athari hizo.
Taswira ya habari imezungumza na baadhi ya wanachi jijini hapa ili kufahamu ni athari zipi wanazozifahamu ambazo zimetokana na biashara hiyo iliyowahi kuikumba Duniani na kuathiri zaidi bara la Afrika .
Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Utamaduni kutoka Wizara ya Habari na utamuduni,sanaa na michezo Dkt. Emanuel Temu anasema kuwa utumwa uliathiri kiasi kikubwa tamaduni za kiafrika pamoja na kudhoofisha maendeleo kutokana na watu kuhamishwa sehemu moja kwenda nyingine.
Kwa zaidi ya miaka 400 zaidi ya watu milioni 15 , wanaume, wanawake na watoto walikuwa waathirika wa biashara hiyo haramu ya utumwa na tarehe ya leo imewekwa na Umoja wa Mataifa kama kumbukizi ya biashara hiyo ikiwa ni fursa ya kuelimisha kuhusu hatari ya ubaguzi wa rangi na chuki zinazoota mizizi katika karne hii.