Zaidi ya Bil.635 zatengwa ujenzi wa barabara nchi nzima
17 May 2021, 12:26 pm
Na; Yussuph Hans
Zaidi ya shilingi Bilion 635 kutoka Mfuko wa Barabara zimetengwa kwa ajili ya matengezo ya Barabara Nchini kwa kipindi cha Mwaka 2021/22.
Hayo yamebainishwa leo bungeni na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mh Leonard Madaraka Chamuriho wakati akiwasilisha hotuba ya mpango wa makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2021/22.
Mh Chamuriho amesema kuwa kwa Mwaka Fedha ujao Wizara imetenga kiasi hicho kwa ajili ya ukarabati huo pamoja na upembuzi yakinifu na ufatiliaji wa miradi hiyo.
Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha wa 2021/22 sekta ya uchukuzi imetengewa zaidi ya shilingi Trilioni 2, kwa ajili ya Matumizi ya kawaida na utekelezaji wa Miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya wizara ya ujenzi na uchukuzi Mh Moshi Selemani amesema kuwa ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo walioyafanya katika kipindi cha mwaka wa fedha uliopita umekuwa na mafanikio makubwa ikiwemo kuongezeka kwa ajira.
Wizara imeomba kuidhinishiwa Tsh Trilioni tatu, bilioni 747, milioni 294, Tisini na Tano Elfu na Mia Mbili, ambapo fedha hizo zimegawanywa katika sekta ya Ujenzi na Uchukuzi kwa Mwaka 2021/22.